Electronic Bibles / Swahili / Swahili Union Bible / Web / Mathayo

Mathayo, Chapter 5

5:1 Naye alipowaona makutano, alipanda mlimani; na alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjia;

5:2 akafumbua kinywa chake, akawafundisha, akisema,

5:3 Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.

5:4 Heri wenye huzuni; Maana hao watafarijika.

5:5 Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi.

5:6 Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa.

5:7 Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema.

5:8 Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu.

5:9 Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu.

5:10 Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.

5:11 Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu.

5:12 Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.

5:13 Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu.

5:14 Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima.

5:15 Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani.

5:16 Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.

5:17 Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza.

5:18 Kwa maana, amin, nawaambia ,Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka,yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka ,hata yote yatimie.

5:19 Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.

5:20 Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.

5:21 Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue, na mtu akiua, itampasa hukumu.

5:22 Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto.

5:23 Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako,

5:24 iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako.

5:25 Patana na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani.

5:26 Amin, nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho.

5:27 Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini;

5:28 lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.

5:29 Jicho lako la kuume likikukosesha, ling'oe ulitupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum.

5:30 Na mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum.

5:31 Imenenwa pia, Mtu akimwacha mkewe, na ampe hati ya talaka;

5:32 lakini mimi nawaambia, Kila mtu amwachaye mkewe, isipokuwa kwa habari ya uasherati, amfanya kuwa mzinzi; na mtu akimwoa yule aliyeachwa, azini.

5:33 Tena mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiape uongo, ila mtimizie Bwana nyapo zako;

5:34 lakini mimi nawaambia, Usiape kabisa; hata kwa mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha Mungu;

5:35 wala kwa nchi, kwa maana ndiyo pa kuwekea miguu yake; wala kwa Yerusalemu, kwa maana ndio mji wa Mfalme mkuu.

5:36 Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kufanya unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi.

5:37 Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu.

5:38 Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa jicho, na jino kwa jino;

5:39 Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili.

5:40 Na mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia.

5:41 Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili.

5:42 Akuombaye, mpe; naye atakaye kukopa kwako, usimpe kisogo.

5:43 Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako;

5:44 lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,

5:45 ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.

5:46 Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?

5:47 Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo?

5:48 Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.