Electronic Bibles / Swahili / Swahili Union Bible / Web / Kumbukumbu la Torati

Kumbukumbu la Torati, Chapter 23

23:1 Aliyejeruhika konde, au aliyekatika tupu yake, asiingie mtu huyo katika mkutano wa Bwana.

23:2 Mwana wa haramu asiingie katika mkutano wa Bwana; hata kizazi cha kumi asiingie aliye wake katika mkutano wa Bwana.

23:3 Mwamoni wala Mmoabi wasiingie katika mkutano wa Bwana; wala hata kizazi cha kumi mtu wao asiingie katika mkutano wa Bwana milele;

23:4 kwa sababu hapo mlipotoka Misri hawakuwalaki na chakula wala maji njiani; na kwa kuwa walimwajiri juu yako Balaamu mwana wa Beori kutoka Pethori iliyo Mesopotamia, aje akuapize.

23:5 Lakini Bwana, Mungu wako, hakukubali kumsikiza huyo Balaamu; Bwana, Mungu wako, aliyageuza yale maapizo kuwa ni baraka, kwa vile alivyokupenda Bwana, Mungu wako.

23:6 Usitafute amani yao wala heri yao siku zako zote, milele.

23:7 Usimchukie Mwedomi; kwa kuwa ni ndugu yako; usimchukie Mmisri, kwa kuwa ulikuwa mgeni katika nchi yake.

23:8 Wana wao watakaozaliwa kizazi cha tatu na waingie katika mkutano wa Bwana.

23:9 Utakapotoka kwenda juu ya adui zako nawe u katika marago, jilinde na kila neno baya.

23:10 Akiwa kwenu mtu awaye yote asiyekuwa ni tohara kwa ajili ya yaliyomtukia usiku, na atoke nje ya kituo, wala asiingie ndani ya kituo;

23:11 lakini na iwe ikaribiapo jioni, yeye ataoga maji; na jua likiisha kuchwa ataingia ndani ya kituo.

23:12 Tena uwe na mahali nje ya kituo, kwa kutokea nje;

23:13 nawe uwe na jembe dogo katika silaha zako; napo uotamapo nje uchimbe kwa lile jembe, na kugeuka na kukifunika kikutokacho;

23:14 kwa kuwa Bwana. Mungu wako, yuatembea katika kituo akuokoe, na kukutolea adui zako mbele yako; kwa hiyo na kiwe kitakatifu kituo chako; asije akaona kitu kwako kisichokuwa safi, akageuka na kukuacha.

23:15 Usimrudishe kwa bwana wake mtumwa aliyejiponya kutoka kwa bwana wake kuja kwako;

23:16 na akae nawe, katikati yako, ndani ya malango yako mojawapo, mahali atakapochagua palipo pema machoni pake; usimwonee.

23:17 Pasiwe na kahaba katika binti za Israeli, wala pasiwe na hanithi katika wana wa Israeli wanaume.

23:18 Usilete ujira wa kahaba, wala mshahara wa mbwa, katika nyumba ya Bwana, Mungu wako, kwa ajili ya nadhiri yo yote; kwani haya ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako, yote mawili.

23:19 Usimkopeshe ndugu yako kwa riba; riba ya fedha, riba ya vyakula, riba ya kitu cho chote kikopeshwacho kwa riba;

23:20 mgeni waweza kumkopesha kwa riba, ila usimkopeshe ndugu yako kwa riba; ili Bwana, Mungu wako, apate kukubarikia katika yote utiayo mkono wako, katika nchi uingiayo kuimiliki.

23:21 Utakapoweka nadhiri kwa Bwana, Mungu wako, usiwe mlegevu katika kuiondoa; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, hataacha kuitaka kwako; nayo hivi itakuwa dhambi kwako.

23:22 Lakini ukijizuia usiweke nadhiri, haitakuwa dhambi kwako.

23:23 Yaliyotoka midomoni mwako yashike kuyafanya; kwa mfano wa ulivyomwekea nadhiri Bwana, Mungu wako, ni sadaka ya hiari uliyoahidi kwa kinywa chako.

23:24 Uingiapo katika shamba la mizabibu la jirani yako, utaweza kula zabibu za kukushibisha, kama upendavyo; ila usitie katika chombo chako.

23:25 Uingiapo katika mmea wa jirani yako waweza kuyapurura masuke kwa mkono wako; ila usisongeze mundu katika mmea wa jirani yako.